Politics

Watoto 70 wakamatwa mtaani katika operesheni Mbeya


By Saddam Sadick

Mbeya. Jumla ya watoto 70 wanashikiliwa jijini Mbeya katika operesheni maalumu iliyofanyika jana Jumatano ya kuwakamata watoto wote wanaozurura mitaani, huku Serikali ikiendelea kuwasaka wazazi wao ili kukabidhiwa.

Akizungumza leo Ahamisi wakati akitoa taarifa ya maandalizi ya kuelekea maadhimisho ya siku ya familia duniani, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema bado utelekezaji wa watoto unaendelea kushamiri.

Amesema ikiwa ni siku tatu pekee zimebaki kuadhimisha siku hiyo, jana wamekamata watoto 70, ambao hawajui wazazi wao walipo na kuitaka jamii kutumia siku kuu hiyo kujitathimini kwenye malezi yao.

“Jana katika operesheni hapa jijini Mbeya tumekamata watoto 70 ambao baadhi utasikia wanasema wana mama hawana baba, wengine wana baba hawana mama, inasikitisha sana,” amesema Homera.

Homera ameongeza kuwa kwa sasa wanaenda kufanya tathimini ya watoto hao ili kujua wenye umri zaidi ya miaka 18 kuweza kuwatafutia shughuli maalumu lakini wakiendelea kuwasaka wazazi wa wale watakaobaki mahabusu.

“Maadhimisho yatafanyika Mei 15 na Mbeya tutasherekea, niwaombe wazazi waliopotelewa na watoto kufika kituo chochote cha Polisi kilicho karibu, lakini tutunze familia zetu,” amesema Homera.

Advertisement

Mmoja wa wananchi katika mtaa wa Uhindini jijini hapa, Jasmine Omary amesema kwa sasa watoto wamekuwa wengi mitaani na haieleweki wanatoka wapi na kushauri kufanyika msako wa nyumba kwa nyuma kuhakiki idadi ya familia.

“Hawa ndio wanakuja kuwa ‘Panya road’ kama tunaowasikia mikoa mingine kwa sababu hawajulikani wanatoka wapi, kimsingi ufanyike msako wa kila nyumba kujua idadi ya watu,” amesema Jasmine.Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published.