Politics

CCM Simanjiro yawaonya madiwani – Mwananchi


By Joseph Lyimo

Simanjiro. Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Amos Shimba amewataka madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kutoingilia uchaguzi wa viongozi wa matawi na kata, akiwasihi kuacha mizengwe na kupanga safu katika uchaguzi huo unaondelea ndani ya chama hicho.

Shimba ameyasema hayo alikuwa anatoa salamu kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo.

Amesema hataki kusikia malalamiko kuwa kuna diwani anafanya mizengwe au kuingilia uchaguzi ili apange safu yake kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

“Huu ni mwaka wa uchaguzi wa CCM kuanzia ngazi ya mashina, matawi, kata, wilaya, mkoa na Taifa, hivyo demokrasia inapaswa kuachwa ili wajumbe wachague kiongozi wanayempenda wenyewe,” amesema Shimba.

Amewataka makatibu na kamati za siasa zinazoratibu uchaguzi huo kumpa taarifa endapo wanapata vikwazo kutoka kwa madiwani wowote wanaowaingilia kazi zao.

Amesema hadi hivi sasa uchaguzi huo unaendelea vizuri na ametembelea maeneo yote ya wilaya hiyo kwa ajili ya kuhakikisha hakuna mizengwe inayofanyika.

Advertisement

“Nilipata malalamiko kidogo kwenye baadhi ya maeneo kuwa makatibu wanawanyima fomu baadhi ya wagombea nikaagiza mtu yeyote mradi ana kadi ya CCM apatiwe fomu na Hilo linatekelezwa,” amesema Shimba.

Amesema kazi ya kukata majina siyo ya katibu wa tawi au kata hivyo fomu zitolewe kwa wagombea bila kuhojiwa maswali ambayo hayahusiani na uchaguzi huo kwani wilaya ndiyo itawajadili na kuwapitisha wagombea.

Diwani wa kata ya Mirerani, Salome Mnyawi amesema diwani hapaswi kuingilia uchaguzi ndani ya chama kwani atakuwa anasababisha makundi yasiyo na maana.

“Diwani hapaswi kupanga safu ili mradi ametekeleza ilani ya uchaguzi wa CCM ipasavyo atachaguliwa na wajumbe wowote bila kupanga safu za kumchagua,” amesema Salome.Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published.